(Waebrania 1, Luka 2, Mathayo 13, Luka 16)
Utangulizi: Je, ulipokuwa shule uligundua kuwa baadhi ya walimu walikuwa wazuri zaidi kuliko wengine? Kwa nini? Tatizo la jumla miongoni mwa waajiriwa wote ni uvivu. Bila shaka baadhi ya walimu ni wavivu, na wanatia juhudi ndogo sana katika kushikilia kazi yao. Walimu wengine wanapenda kufundisha. Wanatia juhudi kubwa kwenye ufundishaji kwa sababu wanapenda kufundisha, na si kwa sababu wanalipwa. Kisha kuna vipengele vya elimu na teknolojia. Je, walimu wamefundishwa mbiu za kufundishia? Je, wanaimudu teknolojia? Mke wangu aliamini kuwa chuo chake hakikumfundisha ujuzi wote wa muhimu wa kufundisha somo la Kusoma. Alimtafuta mwalimu mzoefu kwenye somo hilo na kujifunza kutoka kwake. Mwisho, kuna kipengele cha kibinadamu. Watu wanatofautiana, huku wakiwa na viwango tofauti vya akili, na aina tofauti za vipawa. Vipi kuhusu Yesu? Alijitolea kutufundisha na alikuwa Mungu kamili na mwanadamu kamili – hiyo inamaanisha alikuwa na ujuzi mkubwa wa masuala mbalimbali. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuone kile tunachoweza kujifunza kuhusu Yesu, Mwalimu wetu Mkuu!
I. Mwalimu Bora
A. Soma Waebrania 1:1-2. Ni kwa jinsi gani Yesu ni mwalimu wa hadhi ya juu kwa manabii? (Manabii waliambiwa nini cha kusema. Yesu ni Muumbaji wetu na ni “mrithi wa mambo yote.”)
1. Nilisoma taarifa kwamba mwalimu wa kawaida wa shule ya sheria katika vyuo vya “Ivy League” alikuwa na zaidi ya mwaka mmoja wa uzoefu wa masuala ya kisheria kabla hajaanza kufundisha. Nilipoanza kufundisha katika shule ya sheria nilikuwa nikifanya kazi za kisheria kwa muda wa miaka 30. Hii inaleta tofauti gani ya kiuzoefu kwa wanafunzi? (Ni tofauti kati ya kusoma tu masuala ya sheria na kufanya kazi za kisheria kivitendo. Kwa upande wa Yesu, alitengeneza kila kitu alichokuwa anakizungumzia!)
B. Soma Waebrania 1:3. Yesu ana sifa gani za kutufundisha kuhusu Baba yake? (Kifungu hiki kinasema kuwa Yesu “ni chapa ya nafsi yake.” Tusingeweza kuwa na mwalimu mwenye sifa zaidi ya Yesu. Katika Yohana 14:8 Yesu anatuambia kuwa kama tumemwona, basi tumemwona Baba yake.)
C. Soma 2 Wakorintho 5:14-15. Yesu ni mwalimu mwaminifu kiasi gani linapokuja suala la wanafunzi wake? (Alikufa kwa ajili yetu. Huko ni kujitoa kwa ajili ya ustawi wa wanafunzi!)
II. Mwalimu Anayeendana na Watu
A. Soma Luka 2:11-13. Kwa nini Yesu alizaliwa mahali wanapoishi wanyama?
B. Soma Mathayo 8:20. Kwa nini Yesu hakuwa na makazi? (Ingawa Biblia inatufundisha kuwa matajiri wanakabiliana na changamoto linapokuja suala la kumfuata Yesu, pia inatufundisha kuwa utii kwa Mungu huleta usitawi – hivyo ujumbe unaohusu umiliki wa mali una mchanganyiko. Mara kwa mara huwa kuna chuki dhidi ya matajiri kutokana na dhambi ya wivu. Ninahitimisha kwa kusema kuwa Yesu alikuwa masikini na asiye na makazi ili wanadamu wasimchukie au kudai kuwa hawezi kuendana nasi – bila kujali hali yetu ya kifedha.)
III. Fundisho Jepesi
A. Soma Mathayo 13:3. Tunapata somo gani la kufundisha kwenye maneno, “Akawaambia mambo mengi kwa mifano?” (Visa vinatusaidia kuelewa na kukumbuka jambo linalozungumziwa.)
B. Soma Mathayo 13:4-8. Hebu tuvunjevunje kisa hiki. Mpanzi alishughulikaje na udongo wote? (Udongo wote alishughulika nao kwa usawa.)
1. Je, hilo lilikuwa jambo sahihi?
2. Je, una wazo bora zaidi?
3. Je, mbegu nyingi zilipotea? (Kama kila mojawapo ya mifano hii inahusisha kiasi sawa cha mbegu, basi mbegu nyingi zilipotea.)
4. Je, mbegu zote zilikuwa na mafanikio sawa? (Hapana. Zilitofautiana sana.)
C. Soma Mathayo 13:9. Sote tuna masikio. Ni kitu gani hicho tunachopaswa “kukisikia” kwenye kisa hiki? (Kwa ujumla kisa hiki kinachukuliwa kuwa kinahusu kushiriki (kupeleka) injili na wengine.)
1. Kama ungekuwa unafundisha mambo ambayo Yesu anayamaanisha kwenye kisa hiki, yangekuwa ni mambo gani hayo? (Kuna vigezo vingi vya kuzingatia katika kupeleka injili kwa wengine, vigezo vingi kati ya hivi ni vigumu.)
D. Hebu tupitie tena Mathayo 13:4-5. Kama ungekuwa unaorodhesha changamoto za kufundisha injili, ungeelezeaje jambo hili? (Watu wengine hawako tayari au hawana mazingira mazuri ya kuipokea injili.)
1. Unaona jinsi uelezeaji wa kisa unavyotusaidia kuelewa na kuhifadhi akilini jambo hilo?
E. Hapo kabla nilipokuuliza tunapaswa “kusikiliza” nini, jibu la juujuu ni kwamba hii inahusu matatizo ya kupeleka injili. Tunapata mafundisho gani mahsusi kutokana na kisa hiki? (Wajibu wa mpanzi unatimizwa pale anapogawa mbegu. Anaweza kujaribu kulengesha mbegu yake, lakini vigezo vinginevyo vinaamua mafanikio yake.)
1. Maelfu ya watu wamejiunga ili kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe. Si rahisi kujiunga na mfumo wa kupokea masomo haya, kwa sababu inahitajika uonyeshe nia yako ya kupokea masomo haya mara mbili. Kwa upande mwingine, ni rahisi kuondolewa kwenye orodha ya watu wanaopokea masomo haya – kama mfumo wako wa kompyuta utakataa kupokea somo mara mbili, tayari unakuwa umeondoshwa kwenye orodha. Kwa kulitambua hili kutakufanya udhani kuwa kila mtu aliye kwenye orodha ya kupokea somo anataka kusoma masomo haya. Lakini, hilo si kweli, kiasi cha “wazi” kwa masomo haya kipo chini. Kulijua hili kunakatisha tamaa! Kuna hamasa gani kwenye kisa chetu kumhusu mpanzi?
2. Unadhani kisa cha mpanzi ni rahisi kukielewa? Yaliyokusudiwa ni mepesi kuyaelewa?
IV. Fundisho Gumu
A. Soma Luka 16:1-2. Ungefanya nini kama ungekuwa meneja huyu?
1. Sababu gani imetolewa ya kumfukuza kazi meneja?
B. Soma Luka 16:3-4. Suluhisho gani la kukosa ajira halitafanikiwa kwa meneja huyu?
1. Unadhani suluhisho halitafanya kazi? Au, hataki tu kulikubali?
C. Soma Luka 16:5-7. Hii inaashiria nini kuhusu ukweli wa kumfukuza kazi meneja huyu? (Hii inaonesha uwezekano mkubwa kuwa jambo hili ni kweli. Kwa mara nyingine “anatapanya” mali ya bwana wake. Kibaya zaidi ni kwamba anamfanyia udanganyifu mwajiri wake kwa manufaa yake mwenyewe.)
1. Kutokana na ukweli kwamba meneja alikuwa anajaribu kuangalia mbinu ya jinsi ya kuishi baada ya kufukuzwa kazi, mpango wake ni upi? (Wale wanaodaiwa na mwajiri watajisikia kuwajibika kwa huyu meneja asiye mwaminifu, na watakuwa na mwelekeo wa kumsaidia.)
D. Soma Luka 16:8. Je, kisa hiki ni chepesi kukielewa? (Kama ni chepesi, basi fundisho ni kwamba tunapaswa kuwafanyia udanganyifu watu wengine, hata wale ambao tunawajibika kuwa waaminifu kwao, ili kujinufaisha wenyewe. Hiyo haionekani kuendana na Biblia.)
E. Soma Luka 16:9. Utaona kwamba mfano huu unahusu uzima wa milele, “makao ya milele.” Kama hali ndio hiyo, basi “bwana” ni Yesu na wanadamu wanawakilishwa na meneja. Je, tunapaswa kuwa wezi ili tuweze kulipia mikutano ya injili? Je, hilo ndilo fundisho la mfano huu?
F. Soma Luka 16:10-12. Je, haya ni masikhara? Je, hili ni kosa la tafsiri? Je, Shetani alipenyeza kifungu hiki kwenye Biblia? Kwa nini ujumbe wa kisa uhusu uaminifu wakati kwa dhahiri unatangaza vitendo visivyo vya uaminifu?
G. Hebu turejee nyuma na tuangalie tumekosea wapi. Angalia tena Luka 16:8. Yesu anafikisha ujumbe gani mahsusi? (Ulimwengu una mantiki zaidi kwenye mambo kadhaa kuliko kwa wafuasi wa Yesu.)
H. Soma Luka 16:9. “Mali zisizo za haki” ni kitu gani? (Hizi zitakuwa ni zile ambazo wapagani wanazichukulia kuwa ni mali – fedha, ushawishi, elimu, uzuri, na nafasi.)
1. Sasa, ongezea ujumbe huu kwenye ule uliopo katika kifungu cha 8. Ujumbe mmoja uliounganishwa ni upi? (Yesu anatutaka tutumie mbinu za kidunia zenye mantiki za “kutengeneza marafiki” kwa ajili ya Ufalme wa Mungu. Mantiki inatuambia tutumie fedha zetu, ushawishi wetu, elimu yetu, uzuri wetu, na nafasi yetu ili kuwashawishi wengine kwenye injili.)
I. Soma Luka 16:13. Je, sasa hii inaleta mantiki kama ufupisho wa kisa hiki? (Ndiyo! Yesu anatuhimiza tutumie mali zetu ili kuendeleza wimbi la kuwapata marafiki kwa ajili ya mbingu.)
1. Je, baadhi ya wazee wa kanisa hawaelewi ujumbe huu? (Kama mtu anapendekeza kuwa tunapaswa kufanya mambo kama ambavyo tumekuwa tukiyafanya siku zote, kama mtu anasema kuwa tunapaswa kupuuzia mikakati ya masoko yenye mafanikio, basi mfano huu umelengwa kwa ajili yao.)
J. Rafiki, je, utachukua vidokezo hivi kwa ajili ya kufundishia na kuvijumuisha kwenye uongoaji wako wa roho?
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni