(Zaburi 53, Yohana 1, Ayubu 1)
Utangulizi: Nilipokuwa shule swali kubwa lilikuwa ni, “Unataka kuwa nani? Unataka kusomea taaluma gani katika maisha yako yote?” Katika Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Regent, ambapo ndipo ninafundisha, tunawakabili wanafunzi kwa kuwapa changamoto pana kwa ajili ya mipango yao ya baadaye. Changamoto hii inaitwa “Professional Identity Information.” Unaweza kusema, “Wapo katika Shule ya Sheria, tayari wanalifahamu hilo.” Hapana. “Professional Identity Information” huwapa changamoto ya kujibu swali la “Una mkakati/dira (roadmap) gani kwa ajili ya mustakabali wako? Utakuwa mtu wa namna gani utakapokuwa unatekeleza shughuli za kisheria? Imani yako itayaongozaje maisha yako ya kitaaluma?” Kama ungekuwa unajenga nyumba kwa ajili ya kuishi siku zijazo, je, ungeibuni nyumba hiyo kwa bahati bila kuzingatia utaalamu? Je, utafanya uamuzi wa siku kwa siku juu ya nini cha kufanya? Kimsingi hapana, hutafanya hivyo! Kwa nini basi uchukue njia hiyo kwa ajili ya mustakabali wako? Juma hili somo letu linahusu kile ambacho Biblia inakizungumzia kuhusu mtazamo sahihi wa kidunia wa kuyapangilia maisha yetu na mustakabali wetu. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia!
I. Mlinzi
A. Soma Zaburi 53:1-2. Hii inaashiria nini kuhusu makundi mawili ya watu? (Kuna “wapumbavu” wanaodhani kuwa Mungu hayupo, na hivyo Mungu hazingatii wanayoyafanya. Kisha kuna wale wanaojua kuwa Mungu yupo ambaye anayaangalia matendo yao. Wanatafuta kupata mwongozo wake.)
B. Soma Zaburi 53:3-4. Kuna wapumbavu wangapi? (Kifungu hiki kinasema kuwa wanadamu wote ni wapumbavu.)
C. Soma Zaburi 53:5. Nimesoma habari mbalimbali za tafiti zilizoainisha, hususani miongoni mwa vijana wadogo, hisia za wasiwasi zinazoibuka. Je, kuna sababu ya kuwepo kwa hofu?
1. Kifungu hiki kinaonekana kusema kuwa hakuna sababu ya kuwepo kwa hofu, lakini yote kwa yote watu wanapatwa hofu. Lakini, kifungu kinatoa sababu kubwa ya kuwa na hofu – kwamba Mungu atakudhalilisha, atakuua, na kukunyima mazishi mazuri. Kifungu hiki kinawezaje kusema kuwa hakuna sababu ya kuwepo kwa hofu? (Dhana iliyopo, kwa mara nyingine, ni kwamba kuna makundi mawili. Kwa kundi moja hakuna sababu ya kuwepo kwa hofu kwa sababu hofu haipo. Kwa kundi jingine, wana sababu nzuri ya kuwa na wasiwasi.)
D. Soma Zaburi 53:6. Je, kauli ya awali kwamba kila mtu ni mpumbavu ni ya kweli? Au, je, hiyo ilikuwa ni kutia chumvi? (Kuna watu wanaoweza kufurahi na kufurahia. Hawa ni wale wanaomwamini Mungu na kufundisha habari za Mungu. Jambo la pekee linakuja “kutoka Sayuni!”)
E. Kama ungekuwa umekaa chini ili kutengeneza mkakati/dira kwa ajili ya maisha yako, je, Zaburi 53 ingeathirije mipango yako? (Hakuna mtu anayetaka kuishi kwa hofu. Kila mtu anapenda “shujaa” wa kumwangalia/kumlinda. Mungu anatazama. Mungu anajihusisha na maisha yetu kwa ukaribu kabisa. Mungu ana mpango wa kutenda mambo mema ambayo yataleta furaha na kicheko. Ningependa kuujua mpango huo ili niweze kuufanya uwe mpango wangu!)
II. Uhalisia wa Mlinzi
A. Kwenye kesi, pingamizi mojawapo maarufu ni kwamba swali linakosa “msingi.” Kwa kitendo hicho, mpingaji anamaanisha kuwa dhana zilizomo kwenye swali hilo hazijathibitishwa, na hivyo swali ni batili. Msingi gani unakosekana kwenye maswali/hoja nilizozijenga kwenye kipengele kilichopita katika somo hili? (Kwamba Mungu yupo. Tunaposoma kuwa Mungu anatutazama na kutoa hukumu, hiyo inachukulia dhana gani? Kwamba Mungu yupo.)
B. Soma Yohana 1:1-3. Hii inazungumzia nini kuhusu asili na kuwepo kwa Mungu? (Inasema kuwa “Neno” na “Mungu” walikuwepo hapo mwanzo. Pia inatuambia kuwa Neno na Mungu ni wamoja, na kwamba waliumba kila kitu.)
1. Je, hiyo inatosha kiasi cha wewe kuamini? Vipi kuhusu mwenye kushuku?
C. Soma Warumi 1:19-20. Uthibitisho wetu ni upi kwamba Mungu yupo? (Uumbaji.)
1. Ni kitu gani, kwa mujibu wa vifungu hivi, kwa mahsusi kinamthibitisha Mungu wa uumbaji? (“Uwezo wake wa milele” na “asili yake ya Uungu.”)
2. Fikiria juu ya kile unachokifahamu kuhusu wanadamu tangu enzi na enzi. Je, wengi wao walimwamini Mungu? (Kwa jinsi ninavyoielewa historia, wanadamu wengi tangu enzi na enzi wamekuwa wakimwamini mungu wa namna fulani hivi.)
a. Kwa nini? (Kwa sababu walitambua kuwa wasingeweza kuumba ulimwengu. Walikuwa wanyeyekevu vya kutosha kiasi cha kukubali ukweli huo.)
b. Tafakari jambo hili. Ikiwa bongo zetu zilikua na kugeuka kutokana na bahati na mambo ya asili, kwa nini basi hata tufikirie kuhusu mungu? Mbwa hawafikiri chochote kuhusu miungu. (Ukweli kwamba sisi (na wanadamu wa nyakati zote) tunatafakari suala la “mungu” ni hoja yenge nguvu kimantiki kwenye uumbaji.)
c. Inaonekana kwamba tuna wakanaMungu na agnostiki (wasadikio kuwa hakuna habari za Mungu wala hawawezi kuzijua) kuliko ilivyowahi kutokea kabla katika kipindi ambacho tuna uelewa mkubwa wa ulimwengu. Kwa nini?
D. Soma Warumi 1:21-22. Biblia inatoa ufafanuzi gani kwa wale wasiomwamini Mungu? (Majisifu. Kiburi hiki mwisho wake ni upumbavu uliotiwa giza. Inaonekana dhahiri kabisa kwamba kwa kadri tunavyofunua ugumu wa kila kitu ndivyo ushahidi wa umahiri mkubwa unavyokuwa wa kuvutia zaidi – angalao kwa watu wenye fikra nzuri na yenye mantiki.)
III. Uovu na Mtazamo Wetu wa Kidunia
A. Kama tukiwaambia wapanagi, “Hebu angalia katika maeneo yanayokuzunguka na utamwona Mungu.” Utatarajia jibu gani? (Watakubali, wataonesha uovu wote uliopo, na kusema hii ni hoja yenye nguvu sana dhidi ya kuwepo kwa Mungu mwema.)
B. Soma Ayubu Job 1:6-7. Hii inatufundisha nini kuhusu mfumo wa utawala wa ulimwengu? (Kuna aina fulani ya kamati ya mbinguni inayokutana mara kwa mara.)
1. Nani alikuwa mwakilishi wa dunia yetu katika kipindi hicho? (Shetani.)
C. Soma Ayubu 1:8-11. Hii inaelezeaje mambo mabaya kuwatokea watu wema?
D. Soma Ayubu 1:12. Nani mwenye udhibiti wa mwisho kwenye maisha ya muumini? (Mungu.)
E. Soma Waefeso 6:12-13. Hii inaashiria nini kuhusu maisha ya kila siku? (Kwamba “nguvu za kiulimwengu juu ya giza la sasa” ni vipengele katika maisha yetu!)
F. Unapotafakari mkakati wako kwa ajili ya mustakabali wako, utazingatiaje taarifa hii ya muhimu? (Tunapaswa kutengeneza mkakati/dira, lakini tunatakiwa kuelewa kuwa dirap yetu imewekwa kupitia kwenye ukanda wa mapambano.)
G. Soma Yakobo 4:13-15. Je, Yakobo anatoa ushauri dhidi ya dira kwa ajili ya mustakabali wetu? (Hapana. Anatuonya juu ya hatari ya kutojumuisha mipango ya Mungu katika mustakabali wetu. Dira yetu inatakiwa kujengwa juu ya mapenzi ya Mungu.)
IV. Mtazamo Mpana wa Dira/Mkakati
A. Soma Luka 22:14-16. Hatujajadili injili katika somo hili, lakini ninachukulia kwamba nyote mnaifahamu. Yesu anawaambia nini wanafunzi wake kuhusu mambo yajayo? (Kwamba kuna Ufalme wa Mungu katika siku zijazo.)
B. Soma Luka 22:17-18. Yesu anatuambia nini kuhusu kuila Pasaka na kunywa “mazao ya mzabibu?” (Kwamba atasitisha kuyafanya yote hayo mawili hadi “ufalme wa Mungu utakapokuja.”)
C. Soma Ufunuo 21:1-3. Mustakabali wa waliookolewa ni upi? (Mbingu mpya na nchi mpya ambapo Mungu anakaa pamoja na watu wake.)
1. Je, hii ni sehemu ya dira yako?
2. Kama umesema, “ndiyo,” je, inaathirije uchukuaji wako wa uamuzi sasa hivi?
3. Kama umesema, “ndiyo,” hiyo inaathirije kiwango chako cha wasiwasi katika maisha yako?
D. Rafiki, je, umetafakari mkakati na dira yako kwa maombi mengi? Ni vizuri sana kuwa na dira unapokuwa kijana mdogo, lakini hata wazee wanapaswa kumwomba Roho Mtakatifu kwa ajili ya mwongozo kwa kipindi walichosaliwa nacho hapa duniani. Kulifahamu hili si mwisho wa njia, kwamba njia yetu inaendelea mbinguni, ndio kipengele cha muhimu kabisa cha mpango wetu wa sasa. Je, unaahidi kuifikiria dira kwa dhati kabisa?
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni