Tazama, mimi Paulo nawaambia ninyi ya kwamba, mkitahiriwa, Kristo hatawafaidia neno.
Tena namshuhudia kila mtu atahiriwaye, kwamba ni wajibu wake kuitimiza torati yote.
Mmetengwa na Kristo, ninyi mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria; mmeanguka na kutoka katika hali ya neema.
Maana sisi kwa Roho tunalitazamia tumaini la haki kwa njia ya imani.
Maana katika Kristo Yesu kutahiriwa hakufai neno, wala kutokutahiriwa, bali imani itendayo kazi kwa upendo.
Mlikuwa mkipiga mbio vizuri; ni nani aliyewazuia msiitii kweli?
Kushawishi huku hakukutoka kwake yeye anayewaita ninyi.
Chachu kidogo huchachua donge zima.
10 Nina matumaini kwenu katika Bwana, ya kwamba hamtakuwa na nia ya namna nyingine. Lakini yeye anayewafadhaisha atachukua hukumu yake, awaye yote.
11 Nami, ndugu zangu ikiwa ninahubiri habari ya kutahiriwa, kwa nini ningali ninaudhiwa? Hapo kwazo la msalaba limebatilika!
12 Laiti hao wanaowatia mashaka wangejikata nafsi zao!
13 Maana ninyi, ndugu, mliitwa mpate uhuru; lakini uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo.
14 Maana torati yote imetimilika katika neno moja, nalo ni hili, Umpende jirani yako kama nafsi yako.
15 Lakini mkiumana na kulana, angalieni msije mkaangamizana.
16 Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.
17 Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka.
18 Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria.
19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi,
20 ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,
21 husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.
22 Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,
23 upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.
24 Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake.
25 Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho.
26 Tusijisifu bure, tukichokozana na kuhusudiana.


WAGALATIA 6:1-18

''1 Ndugu zangu, mtu akighafilika katika kosa lo lote, ninyi mlio wa Roho mrejezeni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe.

Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo.
Maana mtu akijiona kuwa ni kitu, naye si kitu, ajidanganya nafsi yake.
Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo atakapokuwa na sababu ya kujisifu ndani ya nafsi yake tu, wala si kwa mwenzake.
Maana kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe.
Mwanafunzi na amshirikishe mkufunzi wake katika mema yote.
Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.
Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele.
Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho.
10 Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio.
11 Tazameni ni kwa herufi gani kubwa nimewaandikia kwa mkono wangu mimi mwenyewe!
12 Wote watakao kuonekana ni wazuri kwa mambo ya mwili, ndio wanaowashurutisha kutahiriwa; makusudi wasiudhiwe kwa ajili ya msalaba wa Kristo, hilo tu.
13 Kwa maana hata wao wenyewe waliotahiriwa hawaishiki sheria; bali wanataka ninyi mtahiriwe, wapate kuona fahari katika miili yenu.
14 Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu.
15 Kwa sababu kutahiriwa si kitu, wala kutokutahiriwa, bali kiumbe kipya.
16 Na wote watakaoenenda kwa kanuni hiyo, amani na iwe kwao na rehema, naam, kwa Israeli wa Mungu.
17 Tangu sasa mtu asinitaabishe; kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake Yesu.
18 Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu. Amina.