Jumatano, 6 Januari 2021

                                           YESU NI NANI KWAKO?


Yesu aliuliza swali kama hili hili kwa wanafunzi wake akisema, 

Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani? Wakasema, Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii.” Mathayo 16:13-14 Kisha Yesu akawauliza wanafunzi wake tena kwamba “Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni.” Mathayo 16:15-17

Fungu hili linasema kwamba Baba ambaye yuko mbinguni amemfunulia Petro kujua kwamba Yesu ambaye alikuwa duniani ni Mwana wa Mungu aliye hai. Wengi hudhani Yesu ni Mungu yuleyule ambaye ni Baba, lakini hapa tunaona Yesu akiwa duniani na Baba akiwa mbinguni na akimfunulia Petro kujua kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu aliye hai; na hii ndiyo sababu mwishoni mwa Injili ya Yohana tunaambiwa kuwa

 “Basi kuna ishara nyingine nyingi alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake, zisizoandikwa katika kitabu hiki. Lakini hizi zimeandikwa ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake.” Yohana 20:30-31

Mahubiri ya kwanza aliyohubiri mtume Paulo baada ya kujifunza Injili kutoka kwa Kristo Mwenyewe, 

“Mara akamhubiri Yesu katika masinagogi, kwamba yeye ni Mwana wa Mungu.” Matendo 9:20. Mtume Petro, ambaye aliishi pamoja na Yesu na kusikia kila kitu kutoka kwake; kwa haraka alisema, “Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.” Yohana 6:69. Wanafunzi wa Yesu pia warikiri kwamba “twasadiki ya kwamba ulitoka kwa Mungu.” Yohana 16:30. 

Martha ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa Yesu, na alisikia mafundisho yake mengi, alisema, “Naam, Bwana, mimi nimesadiki ya kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni.” Yohana 11:27. 

Baada ya Filipo kuhubiri Injili kwa yule towashi, alisema, “Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu.]

” Matendo 8:37. Marko alisema Yesu ni nani katika fungu la kwanza la Injili yake “Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.” Marko 1:1. 

Hata mapepo yalijua “yakapiga kelele, wakisema, Tuna nini nawe, Mwana wa Mungu? Mathayo 8:29. Hivyo, Je, mapepo yalijuaje kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu? Ni kwa sababu yaliwahi kuishi mbinguni kabla shetani hajaangushwa chini (Ufunuo 12:9) na shetani alipodondoshwa chini alikuja na seluthi ya malaika wa mbinguni; hivyo yalimjua Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu. Na hapa lazima tujiulize, kama Yesu angelikuwa ni Mungu Baba, Kwanini hayakusema wazi wazi; mara kwa mara yalisema kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu; na Maandiko yanasema ni kwa sababu yalimjua.

Kristo alisema, 

“Nami nawaambia, Katika wale waliozaliwa na wanawake hakuna aliye mkuu kuliko Yohana Mbatizaji;” Luka 7:28. Yohana Mbatizaji alishuhudia kwamba, “Nami nimeona, tena nimeshuhudia ya kuwa huyu ni Mwana wa Mungu.” Yohana 1:34

Miongoni mwa mashahidi wote, shahidi aliye mkuu kuliko wote ni Baba wa mbinguni. Zaidi ya mara moja aliongea kutoka mbinguni kwamba “Huyu ni Mwanangu mpendwa ninayependezwa naye.” Mathayo 3:17; 17:5.

 Yesu Mwenyewe alitangaza kwamba, “Mimi ni Mwana wa Mungu” Yohana 10:36. Akasema zaidi kwamba, Yeye ni “Mwana pekee wa Mungu.” Yohana 3:18. Kulingana na Biblia, Yesu Kristo alizaliawa, na ni zamani kabla hakijaumbwa kitu chochote, zamani kabla Mungu hajamtuma Yesu kuja duniani (Yohana 3:16-17; 18:37; Wakolosai 1:15; Waebrania 1:1-9 na 1 Yohana 4:9). 

Biblia haijatueleza ni jinsi gani ambavyo Yesu alizaliwa, lakini Mungu anatutaka tujue kwamba Yesu ni Mwanawe anayempenda sana. Yesu alisema, “Maana kama vile Baba alivyo na uzima nafsini mwake, vivyo hivyo alimpa na Mwana kuwa na uzima nafsini mwake.” Yohana 5:26. Kulingana na ushuhuda wake mwenyewe, Yesu ni mzaliwa wa pekee wa Mungu na kwa uhalisi alipokea uzima kutoka kwa Baba yake. 

Hakusema kwamba alikuwa mshiriki wa utatu ambaye anachukua mamlaka yoyote katika utatu; na hivyo Yeye mwenyewe kuwa Baba na Mwana kwa wakati mmoja, bali alisema kuwa Yeye ni Mwana wa Mungu.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

  Yesu Kama Mwalimu Mkuu (Waebrania 1, Luka 2, Mathayo 13, Luka 16)   Utangulizi: Je, ulipokuwa shule uligundua kuwa baadhi ya walimu waliku...