Ijumaa, 15 Januari 2021

 

 Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu 


(Wagalatia 3, Warumi 3, Kumbukumbu la Torati 28)


Utangulizi: Watoto wawili wa kiume walizaliwa siku moja kwenye hospitali moja. Mmoja alikuwa mwanangu na mwingine wa wenzi tuliokuwa tunawafahamu katika jamii yetu. Familia zetu hazikuwa marafiki, lakini tulifahamiana kwa sababu ya rafiki mwingine ambaye sote tulifahamiana naye. Siku moja, watoto wetu walipokuwa na umri wa takribani miaka mitano, mimi na mwanangu tulikuwa tunatembea karibu na shule, wakati huo huo mtoto huyu na baba yake pia walikuwa wakitembea maeneo hayo hayo. Mwanamke mzuri alitupita na kwa mshangao wangu, mtoto huyu wa miaka mitano na baba yake walianza kuujadili mwili wa mlimbwende huyu. Mwanangu hata hakujua kama hili ni jambo la kujadili, achilia mbali kuwa na uelewa wa kutosha kiasi cha kuwa na mawazo ya kuchangia. Tazama jinsi mafundisho ya mzazi yanavyoweza kuleta tofauti kwa maisha ya mtoto! Mungu ni mzazi wetu na sheria yake ni mwalimu wetu. Tunapowafundisha watoto wetu kuhusu sheria ya Mungu, tunapaswa kuiendeaje? Tunapaswa kuwafundisha watoto wetu mtazamo gani kuhusu sheria? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuone kile tunachoweza kujifunza!

 

I.   Sheria Yachunguzwa

 

A.   Soma Wagalatia 3:10. Hebu subiri kidogo! Ikiwa sheria ni mwalimu wetu (kama ambavyo kichwa cha somo kinaashiria), kwa nini basi tunalaaniwa kwa kumtegemea mwalimu wetu?

 

1.   Fikiria mmojawapo wa wanafunzi wangu akielezea: “Ninampenda Profesa Cameron kama mwalimu, lakini kama unautegemea ufafanuzi wake wa sheria uko chini ya laana.”

 

B.   Hebu tujikite kwenye sehemu ya pili ya Wagalatia 3:10. Sababu ya laana ni ipi? Je, ni ufundishaji au kushindwa kufuata mafundisho? (Ni kushindwa kuyafuata. Maneno ya msingi ni kushindwa “kudumu katika yote yaliyoandikwa” na kushindwa “kuyafanya.” Fundisho sio tatizo, bali tatizo ni kushindwa kufuata mafundisho.)

 

1.   Je, hili si dhahiri? Kama ninafundisha darasa la wanasheria watarajiwa, na kama hawajifunzi sheria basi watajikuta kwenye matatizo watakapoanza kuwawakilisha wateja, sawa?

 

2.   Je, uligundua tatizo kwenye swali langu – kifungu kinasema kuyategemea “matendo” ya sheri – tofauti na kuitegemea “sheria.” Matendo ya sheria ni yepi?

 

C.   Soma Wagalatia 3:11. Kwa nini ni “dhahiri” kwamba hakuna ahesabiwaye haki mbele za Mungu kwa sheria? (Kilicho dhahiri ni kwamba hakuna aishikaye sheria. Kama wanadamu wangeweza kuishika sheria kikamilifu, basi kauli hii haiko sahihi, na si ya dhahiri.)

 

1.   Kifungu kinahusianisha kilicho “dhahiri” na “mwenye haki ataishi kwa imani.” Unauelewaje uhusiano huo? (Wenye haki hawaishi kutokana na matendo yao, wanaishi kutokana na imani yao.)

 

D.   Soma Wagalatia 3:12-14. Tutaishije? Kama si kwa kuishika sheria, ni kwa jinsi gani basi? (Kristo ametukomboa kutoka kwenye laana ya kutoishika sheria. Alifanyika laana kwa ajili yetu. Hivyo, kama kifungu cha 11 kinavyosema, “mwenye haki ataishi kwa imani.”)

 

1.   Hebu litafakari jambo hili kidogo. Je, ukweli kwamba hatuwezi kuishika sheria kikamilifu unazungumzia jambo lolote hasi kuhusu sheria? (Hapana. Unazungumzia jambo hasi kutuhusu.)

 

2.   Utaona kwamba kifungu cha 14 kinazungumzia imani yetu na “ahadi ya Roho.” Hii inatufundisha nini kuhusu Roho Mtakatifu? (Haya ni matokeo muhimu ya imani.)

 

a.   Ikiwa unaukana Utatu Mtakatifu, unazungumzia nini kuhusu Roho Mtakatifu?

 

E.   Soma Warumi 3:21. Zingatia sehemu ya mwisho ya kifungu hiki. Ni kwa jinsi gani “Sheria na Manabii wanashuhudia” “haki ya Mungu?” (Kuna majibu kadhaa sahihi, lakini kwa muktadha wetu hii inaonesha kuwa sheria inaendana na haki ya Mungu.)

 

F.   Soma Warumi 3:31. Je, wokovu kwa njia ya imani pekee unamaanisha nini kwenye sheria? (Unaithibitisha.)

 

1.   Hilo linawezekanaje? Kama hatuokolewi kwa sheria, kama hatuwezi kuitii sheria kikamilifu, ni kwa jinsi gani basi tumaini letu kwa Kristo katika kuitii sheria kwa ajili yetu “kunaithibitisha sheria?” (Yesu alikufa, angalao kwa sehemu fulani, ili kuisthibitisha sheria. Kama insingekuwa na umuhimu, Mungu angeifutilia mbali sheria. Asingeshuka duniani na kuzaliwa kama mwanadamu na kuishika sheria kikamilifu.)

 

II.  Sheria Yathibitishwa

 

A.   Soma Warumi 3:20. Ni ipi sababu moja kwa nini sheria ni muhimu sana? (Tunaielewa dhambi kutokana na sheria. Tunaona kile tunachopaswa kukiepuka.)

 

B.   Soma Warumi 3:19. Kuna sababu gani nyingine ya kuwepo kwa sheria? (Inawakomesha wale wanaojisifu kuhusu matendo yao ya haki. Sote hatuna uwezo wa kuishika sheria. Sote “tunawajibika kwa Mungu” kwa dhambi zetu.)

 

C.   Soma Warumi 3:22-24. Je, hii ni habari njema? (Hakuna habari njema kuliko hii! Kushindwa kwetu kuishika sheria ndio sababu ni muhimu sana kuwa na karama ya neema kupitia kile ambacho Yesu ametutendea.)

 

1.   Unapotafakari vifungu vitatu vya mwisho tulivyovisoma, una maoni gani katika kujaribu kuishika sheria? (Sheria ni nzuri. Kushindwa kuishika sheria ndio jambo baya.)

 

D.   Soma Kumbukumbu la Torati 28:1-2 na kisha pitia kwa haraka haraka Kumbukumbu la Torati 28:3-14. Mungu anasema kuwa manufaa ya kuishika sheria ni yepi? (Baraka za aina nyingi!)

 

E.   Soma Kumbukumbu la Torati 28:15 na pitia kwa harakaharaka Kumbukumbu la Torati 28:16-68. Nini kinatokea usipotii sheria ya Mungu? (Mambo ya kutisha! Unanyang’anywa kila kitu.)

 

F.   Hivi karibuni nilisoma “tunawaondolea wanafunzi wetu mambo yasiyosaidia” ili kuwafundisha kuwa wale wanaoishika sheria wanasitawi. Sababu ya kuwa hii ni “kuondoa jambo lisilosaidia” ni kwamba sote tunawafahamu watu wema ambao mambo mabaya yaliwatokea. Kama una mashaka kwamba mambo mabaya yanaweza kuwatokea watu wema, basi soma kitabu cha Ayubu na Waebrania 11. Lakini, hebu tuliweke jambo hili kwenye mtazamo. Je, unadhani kuwa kula vyakula jamii ya karanga vinakufanya uwe na afya nzuri zaidi?

 

1.   Kama umesema “ndiyo,” (na kwa dhahiri ‘ndiyo’ ndilo jibu la kweli), hebu niambia, je, kila mtu anayekula siagi ya karanga anakuwa na afya nzuri? (Kwa mara nyingine, jibu la kweli la dhahiri ni, “hapana,” mara zote unasoma maonyo mengi kuhusu karanga.)

 

2.   Je, kwa kawaida tunaamini kuwa jambo la pekee linabatilisha jambo lililozoeleka? Ukiangalia maisha ya kila mtu unayemfahamu, je, wale wanaoishi kwa kuzingatia sheria ya Mungu wanafanya vizuri au vibaya? Ulinganifu wako uwe ni kwa watu unaowafahamu vizuri. (Wale wanaoifuata sheria ya Mungu wanafanya vizuri zaidi kwa kila namna. Nadhani “haisaidii” kushindwa kufundisha kuwa utii kwa Mungu ndio njia ya kuwa na maisha bora ya hapa duniani na maisha baada ya hapa.)

 

G.   Soma Warumi 1:4-5. Hii inatufundisha kuwa imani huleta nini? (Utii.)

 

1.   Je, hii inaleta mantiki yoyote kwako? (Kama unaamini jambo fulani ni la kweli, kimantiki utaenenda kwa mujibu wa ukweli huo.)

 

2.   Angalia maneno ya mwisho ya Warumi 1:5. Hapa tunaona sababu gani ya muhimu ya kuitii sheria? (“ili mataifa yote wapate kujitiisha kwa imani, kwa ajili ya jina lake.” Tunampa Mungu utukufu kwa kuitii sheria.)

 

a.   Kwa mara nyingine, hebu tulitafakari hili kidogo. Kwa nini utii kwa Mungu humpa utukufu? (Sababu mojawapo ni kwamba humwakisi Mungu vizuri pale unapotii. Unamfanya Mungu ajisikie vizuri.)

 

b.   Je, hiki ndicho tunachokiita “kila upande kupata haki sawa (win, win)?” (Utii hukubariki na humbariki Mungu!)

 

H.   Soma Zaburi 40:8. Je, hii ni kweli kwako pia?

 

1.   Angalia mwendelezo wa sababu za kutii sheria ambazo tumezijadili hadi kufikia hapa. Kwanza, hutufundisha jambo la muhimu sana – hutupatia uelewa wa nini cha kuepuka. Kujua jambo sahihi la kufanya na kulitenda (kwa kadiri inavyowezekana), huleta baraka. Uhusiano kati ya imani yetu na utii wetu huleta mantiki maishani mwetu. Tunaishi maisha ya uaminifu. Hatujisifu kwamba sisi ni bora kuliko jinsi tulivyo kiuhalisia. Maisha ya uaminifu, upendo na yenye tija humpa Mungu utukufu na kututukuza. Mwisho, tunafikia mahali ambapo utii ni kiini cha jinsi tulivyo. Ni jambo la furaha!

 

a.   Uko katika nafasi gani kwenye huu mwendelezo?

 

I.   Soma Waebrania 11:24-25. Hii inatoa onyo gani kwenye taswira ambayo tumekuwa tukiijenga ya utii kwa Mungu? (Tuliligusia hili hapo awali. Utii unaweza (na ndivyo ilivyo) kuleta matatizo ya muda mfupi na dhambi inaweza (na ndivyo ilivyo) kuleta raha ya muda mfupi.)

 

J.   Yumkini kuangalia upande mwingine wa utii itatusaidia kujikita vizuri zaidi kwenye masuala kadhaa. Soma Tito 3:3. Je, ungependelea taswira hii ya maisha? Je, unajiona kuelezewa katika hili?

 

K.   Rafiki, tuna uchaguzi wa wazi. Hatuitii sheria ili kupata wokovu, tunaitii sheria kwa sababu ni baraka kwetu na humpa Mungu wetu utukufu. Je, utamwomba Roho Mtakatifu akuongoze kwenye kila tendo jema?

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

  Yesu Kama Mwalimu Mkuu (Waebrania 1, Luka 2, Mathayo 13, Luka 16)   Utangulizi: Je, ulipokuwa shule uligundua kuwa baadhi ya walimu waliku...